Utangulizi


Kanisa la Usharika wa Ubungo limejengwa kando ya barabara kuu ya Morogoro karibu na kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nyuma ya jengo la UBUNGO PLAZA na limepakana na jengo la RUBADA.

Usharika wa Ubungo kwa sasa una umri unaozidi miaka 36 hivyo nakufanya uwe ni moja ya Sharika kongwe katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani. Usharika huu ulianza kama mtaa wa usharika wa Magomeni mwaka 1969 ukiwa na idadi ya Washarika takriban 10.

Mahali pa kuabudia palikuwa ni chini ya mwembe, sehemu ambayo kwa sasa pamejengwa kituo cha kusambazia umeme (TANESCO). Mwinjilisti wa kwanza alikuwa Mwinjilisti MUNISI. Wakati huo Ibada hazikudumu sehemu hiyo kwa muda mrefu. Washarika walilazimika kuhama sehemu hiyo ili kupisha ujenzi wa Kituo cha Umeme na wakahamia Chuo cha Maji na idadi ya Washarika iliongezeka hadi kufikia 50. Wakati wakiwa Chuo cha Maji, ibada kwa mara nyingine tena ilibidi kuhama baada ya kufukuzwa kutokana na watoto wa SHULE YA JUMAPILI (SUNDAY SCHOOL) waliofanya uharibifu wa kuvunja vioo vya madarasa.

Hivyo ibada katika mwaka 1971 zikahamishiwa kwenye madarasa ya shule ya msingi ya Ubungo National Housing Corporation.

Idadi ya Washarika iliongezeka baada ya kuhamia shuleni kutokana na ukweli kuwa sehemu ya kuabudia ilikuwa na hadhi na kufikia zaidi ya washarika 200. Hili liliwezesha mtaa kupewa hadhi ya kuwa Usharika kamili na hivyo Mchungaji wake wa kwanza alikuwa Mchungaji MLANZI na Mwinjilisti wake wa kwanza alikuwa Mwinjilisti BENJAMIN SHOO. Wakati huo Walutheri na Wamorovian walikuwa wakiabudu pamoja kwa sababu wao nao walikuwa hawajajenga kanisa. Ibada katika shule hiyo hazikudumu kwa sababu serikali ilipiga marufuku shughuli za dini (ibada) kufanywa kwenye madarasa ya mashule, hivyo ilibidi Washarika kutafuta kiwanja cha kujenga kanisa.

Washarika walifanikiwa kupata kiwanja NO:-“437 BLOCK G” UBUNGO na kuanza kujenga mwaka 1972. Mkandarasi wa ujenzi huo alikuwa ITALFRAME ambaye alifanya kazi hiyo na kuimaliza tarehe 1 Juni, 1973. Jengo la kanisa lilifunguliwa rasmi tarehe 21, Aprili 1985,na ASKOFU ELINAZA SENDORO aliyekuwa Askofu wa Sinodi ya Mashariki na Pwani.

Katika mabadiliko ya kutoka kwenye Sinodi kwenda kwenye Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Ubungo ulipangwa kuwa chini ya Jimbo la Dar es salaam na hatimaye Jimbo la Dar es salaam nalo liligawanywa na kuzaa majimbo matatu ambayo ni Jimbo la Temeke, Jimbo la Ilala na Jimbo la Kinondoni.

Hata hivyo mwaka 2009 majina ya majimbo haya yalibadilishwa na Jimbo la Kinondoni likaitwa Jimbo la Kaskazini. Aidha katika uhai wakeUsharika huu wa Ubungo nao umewezesha kuanzishwa kwa Sharika zifuatazo:- Makongo, Usharika wa Kimara, Usharika wa Kibangu, Mabibo External, Usharika wa Msewe, Usharika wa Sinza . Vile vile imewezesha kuanzishwa kwa mitaa ifuatavyo:- Mtaa wa Gide, na Mtaa wa Makoka. Katika mabadiliko yaliyofanyika kuanzia Julai mwaka 2008 Usharika wa Ubungo kwa sasa uko chini ya Jimbo la Kaskazini.