DHAMBI YA KUALIKWA, NI MATESO!

Posted in Mahubiri on Sep 09, 2016


Amri yangu ndiyo hii, mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Yohana 15: 12.

Leo naomba tushirikishane namna ya kuitambua na hivyo kuikimbia „dhambi ya kualikwa.“ Hii ni dhambi ambayo wengi imekuwa ikituondolea upendo baina yetu. Mfano wa dhambi hii ni huu: Mtu anakujia, na kukwambia ubaya wa mtu mwingine; ubaya ambao wewe hujawahi kufanyiwa na mtajwa, wala hujaona mtajwa akimfanyia mtu. Lakini kwa udhaifu wetu au kwa kuogopa kuharibu mahusiano yetu na anayetuletea habari hii, tunaamua kuungana naye, kumchukia mtajwa. Tena wakati mwingine, tunajikuta tunamchukia kupita mleta habari anavyomchukia mtajwa.

Kuna wakati inatokea kuwa tumesimuliwa habari na kumchukia mtu bila hata kumwona. Ila tu moyoni kuna mtu anaitwa Frank, au Juma, au Lucy au Rose tuliyepewa habari zake, na tunayemchukia kwa machungu yasiyo kifani. Mshangao unakuja pale mleta habari amepatana na huyo mtajwa, wakakuacha wewe bado ukimchukia huyo mtajwa. Hii ndiyo dhambi ya kualikwa.

Mpendwa, tuikatae dhambi hii, hata tukisimuliwa habari na mtu tunayemwamini sana. Hatuikatai kwasabau mhusika anasingiziwa au la, bali kwasababu ya agizo la Yesu la Upendo. Tukiona ubaya tunaosimuliwa juu ya mhusika ni kweli, tuchukue hatua ya kumwonya mhusika kwa moyo wa upendo.

Mpendwa wa Yesu, njooni na tupendane kama Yesu alivyotupenda, hata akatufia tungali wenye dhambi. Ubarikiwe na Bwana Yesu.

By Mchungaji