KWANINI TUNATOA LAKINI HATUPOKEI?
Posted in Mahubiri on Jun 20, 2014
Kanuni ya Mungu ni kupokea baada ya kutoa (kupanda na kuvuna). Kuna nyakati tunapanda lakini hatuvuni, Tunatoa lakini hatupokei. Katika hali kama hiyo, tatizo si Mungu, maana “Mungu, si mwanadamu hata aseme uongo” Hesabu 23:19. Bali ni sisi wapandaji/watoaji tunakosea masharti ya kupanda/kutoa. Mungu anasema katika Yakobo 4:3 “Hata mwaomba, wala hampati, kwasababu mwaomba vibaya”. Basi ni lazima na hakika ya kwamba, “tunatoa lakini hatupokei, ni kwasababu tunatoa vibaya” !!
Yafuatayo ni baadhi ya mambo yanayotufanya tusipokee japo tunatoa.
Kwa nini tunatoa lakini hatupokei? – CHECK LIST –
-
Kumwibia Mungu Zaka. (Mal 3:7-12) • Kutoa sadaka wakati unamwibia Mungu zaka, hakuna faida, kwa sababu madirisha ya mbinguni yamefungwa. Sadaka haitazaa. Sadaka yako italeta mavuno mazuri endapo tu madirisha yako ya mbinguni yamefunguliwa kwa zaka unayotoa. Usimwibie Mungu. Toa zaka kwa uaminifu. Utaanza kuona unapokea mavuno (baraka) katika kipimo cha kujaa na kushindiliwa hata kumwagika.
- Kutoa sadaka bila imani (Ebr 11:1,6; Ebr 10:38) “Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo” wengi hutoa sadaka lakini hawana uhakika kuwa ile sadaka itazaa mara 30 au mara 60 au mara 100 (Math 13:3,8)
• Kwa sababu wengi hutoa bila uhakika (imani) sadaka zao haziwi za kupendeza mbele za Mungu. Hivyo hazizai. Kwa sababu hiyo, wanajikuta wanaamini kwamba, ukitoa sadaka, ni kama wamechanga pesa tu, na haitazamiwi kuzaa. Ni kama imepotea. Hayo ni mawazo potofu ambayo shetani amewafanya wengi kuamini hivyo.
• Lakini NENO la Mungu linatupa uhakika (imani) kwa kuwa “imani huja kwa kusikia … Neno la Kristo (Rum 10:17). Mtu akiliamini neno la Mungu, kwamba Mungu hawezi kusema uongo, moyo wake utapokea uhakika (imani). Ndani yake, litajengeka taraja la kupokea, kila anapotoa. Atajua kuwa kutoa sadaka si kupoteza, bali ni kupanda kwa ajili ya mavuno (baraka) kutwa zaidi.
• Kuanzia sasa, pokea uhakika kwamba, ukitoa kwa imani ya kupokea, utapokea. Ukitoa bila imani ya kupokea, hautapokea, utakuwa umechangia tu . Hivyo mbegu haiwezi kuzaa, kwa maana “….kila tendo isilotoka katika imani, ni dhambi” (Rum 14:23)
• Hakuna mkulima anayeweza kutoa kidogo, wakati anaamini mavuno ni mengi. Atoae kidogo hana imani ya kupokea. Anaamini “inapotea”na ndio maana anaona ni bora apoteze kidogo.
• Lakini mwenye imani ya kupokea, hutoa kwa wingi kwa sababu anajua sadaka yake haipotei, bali imepandwa na itazaa sana.
- Kutoa sadaka pungufu ya ile uliyoazimia mwanzo au pungufu ya ile aliyokuongoza Mungu kutoa. (Mdo 5:1-11; Mith 21:27) • Ukipanga moyoni mwako kutoka nyumbani, kumpa Mungu kiasi fulani cha sadaka, baada ya azma hiyo, Mungu anakuwa ameipokea sadaka tayari. Wakati wa utoaji, usipunguze. Laa sivyo utakuwa unamwibia Mungu.
• Watu wengi hukosea kwa kufika ibadani wakiwa wamepunguza sadaka ya Mungu. Katika sadaka hiyo hiyo ananunua gazeti, pipi, au analipa nauli. Hiyo sadaka si takatifu tena. Kwa sababu umeipunguza.
• Panga kutoa sadaka kwa maombi kabisa, uamue kiasi utakachomtolea Mungu na uwe mwaninifu kutokuipunguza, hata iweje. Baadhi ya mikosi itupatayo, ni matokeo ya kumwibia Mungu, kama Anania na Safira .
- Kutoa sadaka kilema Mal 1:13- 14, Walawi 22:20-25 Sadaka kilema ni ile ambayo hata wewe hauihitaji. Ni zile sadaka tunazotoa ili kupunguza mizigo. Mungu hapokei sadaka “reject” (zilizokataliwa) Kamwe, usitoe mabaki (ya dukani, shambani, nyumbani, n.k.) kuwa sadaka, si heshima! Ni laana mbele za Mungu. Mungu hupokea sadaka nono, sadaka nzuri, sadaka bora. “Mheshimu Mungu kwa matoleo yako” *Mith 3:9
• Kama ulichotoa, ndicho pekee kulikuwa kimebaki, Mungu atakipokea vizuri na machoni pake kitakuwa “kinono” hata kama ni kichache, kichakavu au kilema, kwa sababu ndicho pekee ulichobakiza.
-
Kutoa sadaka dhalimu/haramu (Malaki 3:12-13) • Sadaka haramu ni ile iliyopatikana kwa udhalimu, kwa mfano; biashara haramu, dhuluma, rushwa, wizi, uuaji, utapeli, uasi n.k. Wewe ufanyaye mambo ya jinsi hii, ni chukizo mbele za Mungu. Sadaka ya namna hii, haitabarikiwa. Ni haramu. Isa 1:11 –17; Amosi 5:22-27.
- Kutoa sadaka bila upendo wa Kristo ndani yako. (1Kor 13:1-4) • Kama moyo wako unamchukia mtu, jirani, ndugu, au watu wa dhehebu jingine au kabila jingine, haufai kutoa sadaka. Biblia inasema “No profit” (Huna faida)
• Kama umekorofishana na mtu, yakupasa kutengeneza uhusiano wenu kwanza, kabla ya kutoa sadaka.(Math 5:23-25)
• Utoaji ni ibada kamili. Unatakiwa utoe sadaka bila hila, bila kinyongo, bila chuki, bila hasira wala ugomvi au kwazo juu ya mtu. Moyo wako uwe safi. Kama una neno juu ya mtu, “Ungamaneni dhambi ninyi kwa ninyi mpate kuponywa.” (Yak 5:16) • Upendo wa kweli unaunganishwa na amani ya rohoni (Efe 4:1-3) (Ebr 12:14) Mungu anataka tutafute kwa bidii amani (upendo na umoja) ili tupate na baraka zake maishani. Upendo wa kweli, huleta umoja, ambapo Mungu ameamuru baraka zake. (Zab 133:1-3)
-
Kutoa sadaka ili usifiwe (Math 6:2-4; Mith 21-27) • Maana ya andiko hili, sio sadaka yako kuonekana. Bali ni ile nia ya moyoni. Haimaanishi jirani (mkono) yako akiiona sadaka yako, itakuwa batili. Ila kama uliionyesha au uliitaja ili usifiwe, hapo imekuwa batili. Haitakuja na baraka yoyote.
- Kutoa sadaka mahali ambapo hukutakiwa kutoa (Kumb 12:13-14) • Kila sadaka (mbegu) ina mahali pake maalum pa kutolewa (kupandwa). Kuna mbegu hazioti vizuri Ulaya, Afrika, milimnani, mabondeni, mchangani, pwani, majini, n.k.
• Ni muhimu kusikiliza uongozi wa Roho Mtakatifu. Kama sadaka yako Mungu alitaka uitoe kwa yatima, ukiitoa kanisani, utakuwa umekosea. Ni muhimu umuulize Mungu, umsikilize na umtii vizuri. Kuna sadaka za kanisani na za sehemu nyingine nje ya kanisa, kwa mfano; kwa yatima, wajane, masikini, mikutano, semina, safari za watumishi, nyumbani kwa watumishi n.k.
• Tazama Math 13:1-9. Tatizo halikuwa kwa mpanzi, wala katika mbegu zake, bali katika “mahali” mbegu hizo zilipoangukia.
• Si kila udongo, ni udongo tifu-tifu. Udongo tifu-tifu ni pale mahali Roho anakuongoza kutoa. Mahali ambapo kazi ya Mungu inafanyika vizuri kwa utukufu wa Mungu. Mfano:- Kanisani / Mikutanoni, (Mdo 4:36) Wahubiri wa injili (Fil 4:15-20; Gal 6:6). * Kwa Masikini, Yatima, Wajane (Mdo 10:1-4,Isa 1:10-17) • Roho Mtakatifu na akuongoze (Rum 8:14; Yoh 16:13)
-
Kutoa sadaka wakati ambapo hukutakiwa kutoa. (Mhu 3:1-2, 6) Kila jambo lina wakati wake. Hata mbegu, hazipandwi kila siku. Zina majira yake ya kupandwa na kuvunwa. Jifunze kutoa sadaka kwa wakati ambao Mungu anakusukuma kutoa. Msukumo wa Mungu ukija kukugusa kutoa sasa, lakini ukaacha kutii, halafu ukaamua kutoa wiki ijayo, si ajabu usipokee mavuno ya sakaka yako. Kuchelewa kutii ni kutokutii (Late obedience is disobedience). Huwezi kujua, pengine dakika ile ya siku ile, sadaka yako hiyo ilihitajika sana mahali Mungu alipokuwa anakuongoza kutoa. Kwa kutokutii kwako, umekwamisha kazi yake na hutaweza kubarikiwa. (Isa 1:19)
- Kutoa sadaka ili kukubaliwa na Mungu. (Mdo10: 1-6) • Kornelio alidhani Mungu atamhesabia haki kwa wingi wa sadaka na sala zake. Lakini Mungu alimhurumia na akamwonyesha naman sahihi ya kuhesabiwa haki. Yaani wokovu kupitia kwa Yesu Kristo.
• Watu wengi wanatumia sadaka kutafuta haki ya Mungu. Sadaka za hivyo, hazileti baraka. Zinafanana na hongo. Huwezi kumhonga Mungu kwa pesa au maombi. Haki ya Mungu inapatikana bure, kwa toba ya kweli na wokovu kupitia Yesu Kristo. (Mdo 10:17-48) (Efe 2:8-9).
• Toa sadaka kwa moyo safi, kwa nia ya kumwabudu Mungu na kuisukuma injili mbele. Nawe utabarikiwa sana.
• Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, naupendo wa Mungu Baba na Ushirika wa Roho Mtakaktifu, ukae nasi sote, sasa na hata milele, Amina. (2Kor13:14)
NI BORA KUTOKUTOA KABISA. Baada ya kujua kuwa Mungu ana kiwango chake cha kuabudiwa kwa namna ya utoaji wa sadaka, ni muhimu sana ujue haya mambo ili uone faida na baraka za utoaji wa sadaka. Mambo haya yatakusaidia kujipange vizuri kila mara unapotaka kumwabudu Mungu kwa kutoa sadaka.
Ni maombi yangu ukweli huu utajenga desturi ya kuji-check, point kwa point, ili usikosee katika utoaji wako. Hii ni kwasababu, Mungu anapenda UTII (wa maagizo yake/Neno lake) kuliko SADAKA; Ndio maana imeandikwa “Jitunze mguu wako uendapo nyumbani kwa Mungu; Maana ni heri kukaribia ili kusikia kuliko kutoa sadaka ya wapumbavu; ambao hawajui kuwa wanafanya mabaya” Mhubiri 5:1.
NI BARAKA AU LAANA. Kila mara ukamatapo sadaka mkononi, kumbuka kuwa kwa hiyo sadaka, unaweza kubarikiwa au kulaaniwa. Sadaka yako ina nguvu ya kukubariki, kama utatoa vizuri kwa kufuata maagizo ya Mungu; Lakini pia sadaka hiyo ina nguvu za kukulaani, kama utaitoa kiholela bila kufuata utaratibu wa Mungu.
Kwa sadaka hizi hizi, Daudi alibarikiwa, lakini kwa sadaka hizi hizi, Anania na Safira walikufa. Sikia Mungu anachosema. Zishikeni kwa bidii sheria za Bwana, Mungu wenu, na mashuhudiza yake na amri zake alizokuagiza, Nawe fanya yaliyo sawa na mema machoni kwa Bwana, ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kumiliki nchi nzuri Bwana aliyowaapia Baba zako…Tazama, mbele yako kuna baraka na laana, uzima na mauti, chagua uzima upate kuishi. Kumb 6:17-18 “Lakini kueni katika neema na katika kumjua Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo … Heri wakaao nyumbani mwako Bwana, wakuhimidi Daima … Huendelea toka nguvu hata nguvu …na Kila mwenye pumzi, amsifu Bwana … Mheshimu Bwana kwa mali yako, … ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi” (2Pet 3:1 Zab 84:4-5,7 Mith 3:9-10)